KONGAMANO LA TAALUMA ZA MAENDELEO LAANGAZIA MAHITAJI YA DUNIA INAYOBADILIKA

Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na UDOM, SUA, UDSM na MUHAS kimeandaa Kongamano la Tatu la Kitaifa la Taaluma za Maendeleo ili kujadili mwelekeo wa maendeleo ya kijamii yaliyopita, ya sasa na yajayo, ili kukidhi mahitaji ya dunia inayokabiliwa na changamoto za teknolojia na mabadiliko ya tabianchi.

Akifungua rasmi kongamano hilo leo tarehe 10 Disemba 2024, Mjini Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia upande wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel E. Mushi aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa vyuo vikuu vina jukumu kubwa la kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za kisasa. “Ni lazima tuwafundishe vijana wetu siyo tu maarifa bali pia ujuzi wa kutatua changamoto za maendeleo kwa lengo la kuibadilisha jamii,” alisema Prof. Mushi.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amewaasa washiriki wa kongamano hilo kuzingatia kasi ya mabadiliko ya teknolojia na tabianchi. “Taaluma za maendeleo lazima zilingane na kasi ya mabadiliko duniani, ni jukumu letu kama vyuo vikuu kuhakikisha tunatoa maarifa yatakayosaidia jamii kukabiliana na changamoto hizi,” alisisitiza Prof. Mwegoha.

Kwa upande wake, Prof. Elizabeth Lulu Genda, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo Chuo Kikuu Mzumbe, alibainisha kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kujadili mchango wa taaluma za maendeleo katika kuboresha maisha ya watu. “Mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, na kimazingira yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya vyuo vikuu, watafiti, na wadau wa maendeleo ili kutoa suluhu zenye tija,” alisema Prof. Genda.

Mada elekezi katika kongamano hilo ziliwasilishwa na Prof. Maia Green kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza, ambaye alitoa mada yenye mtazamo wa kimataifa kuhusu maendeleo ya kijamii na teknolojia na Dkt. Colman Msoka, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Maendeleo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alijikita katika kuonyesha njia bora za kuboresha uhusiano kati ya utafiti wa maendeleo na mahitaji ya kijamii ya Tanzania.

Aidha washiriki walipata nafasi walijadili kwa undani masuala muhimu kupitia mijadala sambamba na kuwasilisha tafiti ili kupitiwa na kuboreshwa kabla ya kuchapishwa Kongamano hili limeweka msingi wa mabadiliko muhimu katika taaluma za maendeleo kwa kuhakikisha mawasiliano ya karibu kati ya watafiti, serikali, na wadau wa maendeleo. Hii ni hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu nchini Tanzania.

**************

 

Contact Us

Vice Chancellor,

Mzumbe University,

P.O.BOX 1,

Mzumbe, Morogoro.


Tel: +255 023 2604380/1/3/4
Fax: +255 023 2931216
Cell: +255 0754 694029
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.