Aliyosema Profesa William Mwegoha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe
# Mwaka huu 2024 Chuo Kikuu Mzumbe kinaweka historia kwa kutoa shahada ya udaktari wa heshima ya kwanza na kwa pekee kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni muhitimu wa chuo hiki mwaka 1986.
#Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe inakupongeza kwa kazi unayofanya kama kiongozi wa nchi hii, chuo hiki kinajitanabaisha kuhusika moja kwa moja katika kujenga msingi wa heshima kubwa unayoendelea kuipata kutokana na uongozi wako katika nchi hii na Duniani kwa ujumla.
#Kwa upande wa taaluma, katika mwaka 2023/2024, chuo kilisajili jumla ya wanafunzi 15,086 katika ngazi ya astashahada hadi shahada ya uzamivu katika kampasi zote tatu, katika hao wanawake ni 7, 342 na wanaume 7,744 baadhi yao ndio hawa unaowaona leo katika mahafali haya.
#Chuo kimeendelea na kuwaajengea uwezo wahadhiri wetu ili wasimamie kazi za wanafunzi kwa umahiri, na uzamivu kwa ufanisi ili kuhakikisha wanafunzi wanakamilisha kazi zao kwa wakati na kufanya tafiti bora na matokeo yake tumeanza kuyaona, ambapo leo tuna wahitimu kwa mara ya kwanza, shahada za uzamivu 12 idadi ambayo ni rekodi kwa Chuo Kikuu Mzumbe.
Aliyosema Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda
#Natoa pongezi kwa uongozi wote wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa mahafali haya mazuri sana, pia nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kikanuni mlioufanya wa kutoa udaktari wa heshima katika uongozi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
#Udaktari wa heshima anastahili kwa kazi anayoifanya, lakini najua mnajivunia vile vile kwamba yeye nae alipitia hapa, uamuzi huu ni sahihi sana, kwa nafasi aliyo nayo na kazi aliyoifanya nchini, Mhe. Rais anastahili sana.
Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
#Nalishukuru Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe kwa uamuzi wake wa kunipa heshima na kunitunuku Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uongozi.
#Nafarijika kwamba shahada hii leo inatolewa na chuo kilichonijengea misingi ya kuwa kiongozi katika taifa hili.
#Nina furaha kwamba pamoja na shahada niliyopokea leo, namshukuru Mungu kwamba, nimeshapokea shahada nyingine tano za udaktari wa heshima kutoka vyuo mbalimbali nchini na duniani, nimepokea kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India, Chuo Kikuu cha Sayansi za Siasa cha Uturuki, Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Anga Korea. Hii ni shahada ya sita, nami nimesimama hapa kwa unyenyekevu mkubwa, kukubali heshima hii niliyopewa na Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi kuu ya Morogoro, asanteni sana, nashukuru sana.
#Kutambuliwa na chuo chenye historia ya kuwa tanuri la kuoka viongozi wa taifa hili, ni heshima kubwa sana, najisikia fahari kwamba chuo kilichonijenga na kunitayarisha kuwa kiongozi kimetambua kazi yangu na leo hii kinanitunuku shahada ya heshima
#Kwa kuwa suala la uongozi lina mchango wa watu mbalimbali, naitoa shahada hii ya heshima kama zawadi kwa wote wenye mchango kwenye maisha yangu kiuongozi, akiwepo Mkuu wa chuo hiki, Rais Mstaafu Dkt. Ali Mohammed Shein, kwani yeye ni mmoja kati ya walezi na aliyenifinyanga kuwa nilivyo leo, lakini pia wakiwemo wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
#Nchi yetu imetimiza zaidi ya miongo 6 ya kujitawala, mimi ni Rais wa 6 katika kuitumikia nchi yetu, baada ya Baba wa Taifa aliyefanya kazi kubwa ya ukombozi na kuweka misingi madhubuti ya kuongoza Taifa letu, alifuatiwa na viongozi mahiri ambao katika vipindi vya uongozi wao walitoa mchango mkubwa na kila mmoja kumwachia anayemfuata misingi imara ya kuendeleza taifa letu kisiasa, kiuchumi na kijamii
#Kila awamu ya uongozi ilikuwa na mchango mkubwa wa taifa letu kuwa lenye utawala bora, utulivu wa kisiasa, na uchumi unaoeleweka kwa nyakati husika, vile vile wameendeleza amani na mshikamano.